Uchaguzi mdogo wa Ol Kalou mtihani kwa IEBC

Martin Mwanje
2 Min Read
Erastus Ethekon - Mwenyekiti wa IEBC

Uchaguzi mdogo unaoandaliwa katika eneo bunge la Ol Kalou leo Alhamisi umeiweka Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwenye mizani. 

Upinzani unasema utatumia uchaguzi huo kupima ikiwa tume hiyo inayoongozwa na Erastus Ethekon ina makali ya kutosha kuandaa uchaguzi mkuu huru, wa wazi na haki mwaka 2027.

Tayari, wapinzani wameikosoa tume hiyo kwa kushindwa kutema visa vya utoaji rushwa na vurugu vilivyoshuhudiwa wakati wa kampeni katika eneo bunge la Ol Kalou.

Isistoshe, kinara wa chama cha DCP Rigathi Gachagua ameelezea mashaka yake na utendaji kazi wa tume hiyo akidai inaegemea mrengo wa Kenya Kwanza.

Ni madai ambayo IEBC imeyapuuzilia mbali na ikiyataja kuwa yasiyokuwa na msingi.

Ingawa timu ya Erastus Ethekon imefanya chaguzi kadhaa ndogo ikiwa ni pamoja na katika maeneo bunge ya Kasipul Kabondo, Mbeere Kaskazini na Malava, haijawahi kusimamia uchaguzi mkuu ambao kwa kawaida huwa na ushindani mkali na matarajio makubwa, hususan kinyang’anyiro cha urais.

Tume hiyo mpya ya IEBC ilikula kiapo cha utendaji kazi mwezi Julai mwaka 2025.

Inajumuisha Ethekon ambaye ni mwenyekiti wakati Fahima Araphat Abdallah akihudumu kama naibu mwenyekiti.

Makamishna wanajumuisha Prof. Francis Odhiambo Aduol ambaye wakati mmoja alihudumu kama Makamu Chansela wa Chuo Kikuu cha Kiufundi cha TUK, Ann Nderitu ambaye wakati mmoja alihudumu kama Msajili wa Vyama vya Kisiasa na Dkt. Alutalala Mukhwana.

Makamishna wengine ni Mary Sorobit na Hassan Noor Hassan.

Tume hiyo imeahidi kuwa itafanya kila iwezalo kuhakikisa uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 utakuwa wa huru na wa haki.

Upinzani unasema ahadi hiyo itadhihirika tu kwa namna itakavyoendesha uchaguzi mdogo wa Ol Kalou huku ikiwa imesalia takriban miezi 13 kabla ya uchaguzi mkuu ujao kuandaliwa.

Hata hivyo, IEBC imeonya dhidi ya utoaji wa taarifa zinazoweza kuondoa imani ya umma katika utendaji kazi wake.

Share This Article