Wakazi wa Ol Kalou wapiga kura kumchagua mbunge mpya

Vituo vingi vya kupigia kura vilifunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na vitafungwa saa kumi na moja jioni.

Martin Mwanje
2 Min Read

Wakazi wa Ol Kalou wapatao 73,480 waliojisajili kama wapiga kura leo Alhamisi wanapiga kura kumchagua mbunge wao mpya atakayewawakilisha bungeni kwa kipindi kilichosalia kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027. 

Foleni ndefu za wapiga kura zimeonekana katika vituo vingi vya kupigia kura ikiwa ni ishara kwamba wakazi wanafahamu ushindani mkali uliopo kwenye kinyang’anyiro hicho.

Mgombea wa UDA Muchina Nyagah tayari amepiga kura katika shule ya msingi ya Huruma.

Mgombea wa DCP Sammy Ngotho anatarajiwa kupiga kura katika shule ya msingi ya AC.

Vituo vingi vilifunguliwa majira ya saa kumi na mbili asubuhi na vitafungwa majira ya saa kumi na moja jioni.

Kwa vituo vile vilivyofunguliwa kuchelewa, muda huo utafidiwa kwa kukawia kuvifunga.

“Muda wowote uliopotea wakati wa kufunguliwa kwa vituo vya kupigia kura utafidiwa wakati wa kufunga vituo hivyo. Wapiga kura wote walio kwenye foleni kufikia saa kumi na moja jioni wataruhusiwa kupiga kura,” ilisema Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwenye taarifa awali.

Eneo bunge la Ol Kalou lina vituo 144 vya kupiga kura.

Upigaji kura unaendelea wakati maafisa wa usalama zaidi ya 1,000 wakishika doria kuhakikisha hakuna hata chembe ya nuksi wakati wa mchakato wa kupiga kura.

Ili kupiga kura, ni lazima mtu awe na kitambulisho chake halisi cha kitaifa au pasipoti halali ya Kenya.

Mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon ameashiria kuwa hakuna mwanasiasa, haijalishi ni mwandamizi kiasi gani, ataruhusiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura na mawakala au wafuasi ambao hawajaidhinishwa na tume hiyo.

Lengo ni kuhakikisha hakuna vurugu zitatokea na hivyo kutatiza mchakato wa kupiga kura.

Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja kwa upande wake ameashiria kuwa amewatuma maafisa zaidi ya 1,000 kuhakikisha usalama wa kutosha wakati na baada ya kupiga kura.

Uchaguzi mdogo wa Ol Kalou unaandaliwa kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa eneo hilo David Njuguna Kiaraho mwezi Machi mwaka huu.

Ingawa kuna jumla ya wagombea 9 kwenye uchaguzi huo mdogo, ushindani mkuu ni kati ya mgombea wa UDA Muchina Nyaga na Sammy Ngotho wa DCP.

Share This Article