Afisa wa zamani wa jeshi Meja Peter Mwaura Mugure leo Jumanne amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Nyeri Martin Muya alimhukumu Mugure kifungo hicho kwa kumuua mkewe na watoto wao wawili.
Hii ni baada ya afisa huyo kupatikana na hatia katika mashtaka yote matatu ya mauaji.
Jaji Muya alisema makosa hayo yalistahili adhabu kali.
Katika kufikia uamuzi huo, mahakama ilizingatia athari ya taarifa ya familia ambayo ni waathiriwa na ile ya upande wa mashtaka ulioongozwa na viongozi wakuu wa mashtaka Jennifer Kaniu na Pithon Mwangi.
Wote hao walitaka Mugure ahukumiwe kifungo cha maisha.
Jaji Muya alisema mshtakiwa hakuonyesha hata chembe ya kujutia matendo yake wakati wa kipindi cha kesi hiyo akisema ongezeko la visa vya mauaji ya watoto na wanawake linahitaji adhabu kali.
Upande wa mashtaka ulibaini kuwa Mugure, ambaye wakati huo alihudumu kama meja katika Kambi ya Anga ya Laikipia, aliishawishi familia yake kwenda kwenye kambi hiyo kwa kisingizio cha kutembelewa na familia.
Kisha Oktoba 26, 2019, aliwaua watoto wake wawili na mama yao.
Mugure alificha miili ya watatu hao kwenye buti ya gari lake na kuisafirisha hadi katika eneo la mbali ilikotupwa miili hiyo.
Mashahidi kwenye kesi hiyo walisema Mugure alitembelea eneo ilikotupwa miili hiyo siku tatu kabla ya mauaji hayo na kisha kuchimba kaburi lenye kina kifupi kuashiria alipanga kutekeleza mauaji hayo.