Serikali imeanza ujenzi wa zaidi ya kilomita 400 za barabara za thamani ya shilingi bilioni 25 katika kaunti ya Nyandarua, kama sehemu ya juhudi zinazolenga kuimarisha miundombinu na usafiri katika eneo hilo.
Waziri wa uchukuzi na barabara Davis Chirchir, alitangaza miradi hiyo wakati wa ziara ya ukaguzi na uzinduzi wa barabara ya Ngorika–Kanjuiri yenye umbali wa kilomita-37.
Waziri huyo alithibitisha kuwa Serikali Kuu imelipa madeni yaliyokuwa yakidaiwa na wanakandarasi ya shilingi bilioni 175, hatua aliyosema itafanikisha ukamilishaji wa miradi ya miundombinu kote nchini.
Aidha, alipuzilia mbali uvumi kwamba miradi inayotekelezwa katika kaunti ya Nyandarua, imeshawishiwa na uchaguzi mdogo ujao wa ubunge katika eneo bunge la Ol Kalou, akidumisha kuwa miradi husika ni sehemu ya ajenda ya maendeleo ya muda mrefu ya serikali.
“Miradi hii itatoa fusa ya masoko kwa wakulima wetu, itaimarisha usalama barabarani, itawezesha kufikiwa kwa mashule, hospitali na huduma zingine za serikali, huku ikitoa nafasi za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi,” alisema Chirchir.