Ujerumani yaipa Kenya shilingi bilioni 7.8 kufadhili miradi yake

Ufadhili huo ulipatikana wakati wa mkutano kuhusu maendeleo ya ushirikiano  kati ya serikali hizo mbili,  Jijini Berlin.

Tom Mathinji
1 Min Read
Kenya yapokea shilingi bilioni 7.8 kutoka Ujerumani.

Kenya imepokea shilingi bilioni 7.8 kutoka serikali ya Ujerumani, kufadhili miradi mbalimbali katika muda wa miaka miwili.

Ufadhili huo ulipatikana wakati wa mkutano kuhusu maendeleo ya ushirikiano  kati ya serikali hizo mbili,  Jijini Berlin.

Katibu wa Hazina Kuu Dkt. Chris Kiptoo, alisema ufadhili huo utapiga jeki ukuaji wa sekta ya kibinafsi, biashara na uwekezaji, mabadiliko ya kidijitali, elimu ya kiufundi, nishati mbadala, unyunyiziaji maji mashamba, mifumo ya chakula na uongozi bora.

“Pia tunakaribisha ishara kwamba tutapata shilingi bilioni 4 zaidi kupiga jeki sekta ya nishati katika muda wa majuma kadhaa yajayo,” alisema Kiptoo.

Mkutano huo wa siku mbili, pia ulilenga kuimarisha ushirikiano katika kilimobiashara na upatikanaji wa soko, leba kupitia ujuzi wa kiufundi na upanuzi wa mafunzo ya lugha, ukuaji wa nishati mbadala, uchukuzi kutumia umeme na uwekezaji.

Deta rasmi zinadokeza kuwa mauzo ya Kenya nchini Ujerumani yameongezeka kwa asilimia 75, kutoka dola milioni 203 mwaka 2021, hadi dola milioni 352 mwaka 2025.

“Ili kupanua fursa hizi, serikali ya Kenya imejitolea kutatua vikwazo vinavyohusiana na upatikanaji wa soko, mikakati ya udhibiti na uchukuzi,” aliongeza Kiptoo.

Share This Article