Rais William Ruto amesema biashara ndogo ndogo na zile za kadri ni muhimu kwa ukuaji wa uchumi wa taifa hili, huku zikichangia asilimia 40 ya pato jumla la taifa (GDP).
Akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Biashara ndogo ndogo na za Kadri Duniani, Rais alisema nchini Kenya asilimia 98 ya biashara zote ni zile ndogo ndogo za kadri ambazo zinatoa asilimia 90 ya fursa za kazi ambazo sio za kilimo.
“Kwa hivyo tunapozungumza kuhusu mustakabal wa kiuchumi wa kenya, tunazungumza kuhusu biashara ndogo na za kadri (MSMEs). Ufanisi wa biashara hizo ni ufanisi wetu,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi wa taifa aliwasihi vijana kutumia fursa ya kushuka kwa gharama ya kusajili biashara kufanya biashara zao kuwa rasmi.
Rais Ruto aliongeza kuwa ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo, serikali ilileta hazina ya Hustler ambayo imetoa zaidi ya shilingi bilioni 90 kwa zaidi ya Wakenya milioni 27, na kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 6 kama akiba kutoka kwa wananchi.
“Tumegeuza miradi ya serikali kuwa masoko ya MSMEs,” aliongeza kiongozi wa taifa.
Wakati huo huo Ruto alisema taifa hili linakabiliwa na nakisi ya ufadhili wa kifedha wa MSME ya shilingi trilioni 3.
“Changamoto hilo sio la kipekee nchini Kenya. Benki ya Dunia inakadiria kuwa biashara ndogo ndogo katika mataifa yanayostawi yanakabiliwa na nakisi ya ufadhili ya dola trilioni tano za kimarekani.
Sherehe hiyo ya Siku ya Biashara ndogo ndogo na za Kadri Duniani, iliadhimishwa katika Jumba la Mikutano ya Kimataifa (KICC), Jijini Nairobi.