Muda wa utekelezaji wa 8% ya VAT kwenye bidhaa za petroli waongezwa

Martin Mwanje
1 Min Read
Opiyo Wandayi - Waziri wa Nishati

Serikali ya Kenya Kwanza imeongeza kwa kipindi cha miezi mitatu muda wa utekelezaji wa ushuru thamani wa ziada (VAT) kwenye bidhaa za petroli humu nchini. 

Waziri wa Nishati Opiyo Wandayi anasema kipindi cha utekelezaji wa ushuru huo sasa kitaendelea hadi Oktoba 14 mwaka huu.

“Zaidi ya hayo, katika kipindi cha kutangazwa kwa bei mpya cha mwezi Julai hadi Agosti mwaka 2026, serikali itatumia ruzuku kutoka kwa Ushuru wa Maendeleo ya Petroli hadi kima cha shilingi milioni 945 ili kumudu viwango vya sasa vya bei,” aliongeza Waziri Wandayi wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumanne.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inalenga kuwalinda Wakenya dhidi ya bei za juu za mafuta zinazotokana na mzozo unaoendelea katika Mashariki ya Kati na pia kuunga mkono biashara na kulinda uchumi wa taifa dhidi ya athari kutoka nje ya nchi.

Waziri Wandayi amewahakikishia Wakenya kuwa bado kuna mafuta ya kutosha nchini licha ya mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati kusababisha bei za mafuta kuanza kupanda tena.

Usafirishaji wa bidhaa hiyo muhimu duniani umeathiriwa tena kutokana na kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz wakati Marekani na Iran zikianza kushambuliana tena.

Share This Article