Gavana Otuoma awahakikishia wafanyabiashara wa Busia usalama wao

radiotaifa
1 Min Read
Paul Otuoma - Gavana wa Busia

Gavana wa kaunti ya Busia Dkt. Paul Otuoma amewahakikishia wafanyabiashara katika mji wa Busia mazingira salama ya kufanyia kazi kufuatia wiki kadhaa za ukosefu wa usalama uliotatiza biashara mjini humo. 

Amesema utawala wake unafanya kazi kwa karibu na asasi za usalama kurejesha utulivu na kulinda biashara.

Aidha, amesema utawala wake umedhamiria kuangamiza shughuli za kiuhalifu na kuhakikisha wafanyabiashara wanaendelea na shughuli zao bila uoga.

Gavana huyo aliyezungumza mjini Busia wakati wa mkutano na wafanyabiashara na wadau wengine wa biashara, alitaja mazingira salama kuwa muhimu kwa ukuaji wa uchumi na uwekezaji.

Wakiongozwa na James Nyongesa, wafanyabiashara hao walifurahia hakikisho la Gavana huyo ila wakatoa wito wa operesheni endelevu za usalama ili kuhakikisha kuna usalama wa kudumu.

Taarifa ya Sayyid Abdalla 

 

Share This Article