Wazee wa Kaya wa jamii ya Mijikenda wamemkosoa vikali aliyekuwa Waziri, Chirau Ali Mwakwere, kwa kushirikiana na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua na kujitangaza kuwa msemaji wa jamii hiyo.
Walisema kuwa Mwakwere sio msemaji wa jamii ya Mijikenda na kwamba anamuunga mkono Gachagua binafsi kwa manufaa yake mwenyewe, wala hawakilishi maslahi ya jamii ya Mijikenda.
Haya yanajiri siku chache tu baada ya Gachagua kufanya mkutano na wazee wa jamii ya Mijikenda wakiongozwa na Mwakwere.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika Kaya Fungo Giriama, eneo la Kaloleni, Kaunti ya Kilifi, wazee hao pia walimtuhumu Gachagua kwa kupanga njama za kuigawa jamii ya Mijikenda na kuapa kuwa hawataruhusu jambo hilo kutokea.
Walisema jukumu lao ni kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa jamii yao, na kwamba kwa sasa wanaunga mkono kikamilifu utawala wa Rais William Ruto kwa kuwa unaendelea kushughulikia dhuluma za kihistoria za ardhi na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo Pwani.
Mwakilishi wa vijana katika chama cha Wazee wa Kaya wa Mijikenda, Nguma Charo, alisisitiza kwambajamii ya Mijikenda inaunga mkono kikamilifu Rais William Ruto, na kwamba kosa alilofanya Mwakwere ni kujitangaza kuwa msemaji wa jamii hiyo ilhali si kweli.
“Tulimwita hapa kama wazee na tukampa siku 14 kuomba radhi kwa wazee, lakini hakufanya hivyo kwa sababu yeye sio msemaji wa Mijikenda,” alisema.
Mzee wa Kaya, Shungu Thuva, alisema kuwa kiongozi yeyote anayehitaji ushirikiano na jamii ya Mijikenda anapaswa kushirikiana na Wazee wa Kaya badala ya mtu mmoja mmoja kama Mwakwere.
Hamisi Juma, ambaye pia ni Mzee wa Kaya wa Mijikenda, alisema wanahitaji kukutana na Rais kumweleza shida zao ambazo viongozi wa Pwani hupuuza kila mara wanapomkaribisha Rais.