Shirika la Ndege la Air France, limesimamisha kwa muda safari zake za kuingia na kuondoka Kinshasa, baada ya abiria mmoja aliyesafiri kutoka Kinshasa hadi Jijini Paris kugunduliwa kuwa na ugonjwa wa Ebola.
Kupitia kwa ilani kwenye mtandao wake, shirika hilo lilisema safari zilizositishwa zitaathiri huduma zinazotolewa Jijini Kinshasa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), likisema linajizatiti kuhakikisha linarejesha safari hizo haraka iwezekanavyo.
Wakati huo huo, Air France ilisema inashirikiana kwa karibu na Mamlaka za Afya nchini DRC kuimarisha uchunguzi wa wasafiri kabla ya kuabiri ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kinshasa airport.
Shirika hilo lilisema linawasaidia abiria walioathiriwa na kusitishwa kwa safari hizo, kuhakikisha wanapanga upya safari zao.
Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Wizara ya Afya ya Ufaransa kuthibitisha kisa cha Ebola kilichomhusisha mhudumu wa afya ambaye alikuwa akirejea kutoka DRC.
Kupitia kwa taarifa Juni 24, serikali ya DRC ilisema imepokea taarifa hiyo, ikisema mwathiriwa alikuwa daktari aliyekuwa akifanya kazi katika kitengo cha kukabiliana na Ebola.
Visa 1,155 vya Ebola vimethibitishwa, vifo 304 kunakiliwa huku wagonjwa 326 wakitangazwa kupona virusi hivyo nchini DRC.