Lemayan atetea taji ya mbio za marathoni za Lewa Safari

Katika mbio za kilomita 42 wanawake, Lidyia Simiyu alitawala kutoka mwanzo na kukata utepe kwa  muda wa saa  mbili dakika 50 na  sekunde 39.

radiotaifa
2 Min Read

Samson Lemayan ametetea taji ya mbio za marathoni za Lewa Safari,huku Lydia Simiyu akitwaa ubingwa kwa wanawake katika makala ya 26 yaliyoandaliwa Jumamosi katika hifadhi ya wanyamapori ya Lewa,kaunti ya Isiolo.

Lemayan ambaye ni afisa wa shirika la wanyamapori nchini (KWS), alizikamilisha mbio hizo kwa muda wa saa mbili dakika 27 na sekunde 4, akifuatwa na Victor Miano na Nehemiah  Kimaru waliotwaa nafasi za pili na tatu mtawalia.

“Ninafurahi kutetea ubingwa wangu. Njia ilikuwa ile ile na hali ya hewa pia ilikuwa ile ile. Nasubiri maelekezo kutoka kwa meneja wangu kuhusu mashindano nitakayoshiriki baadaye. Ninashiriki Lewa Safari Marathon kwa sababu ni mashindano makubwa, hasa kwa jamii ya wahifadhi na kwangu kama askari wa uhifadhi. Ushindi huu ni mahususi kwa familia yangu na mashabiki wangu,” alisema Lemayan.

Katika mbio za kilomita 42 wanawake, Lidyia Simiyu alitawala kutoka mwanzo na kukata utepe kwa  muda wa saa  mbili dakika 50 na  sekunde 39,akifuatwa na  Lydia Nyansikera katika nafasi ya pili , huku bingwa wa makala ya mwaka jana  Gladys Otera, akimaliza wa tatu.

“Ninamshukuru Mkurugenzi Mkuu wa KWS kwa kunipa fursa ya kufanya mazoezi na kwa msaada ulionifanya niweze kushiriki na kushinda leo. Ushindi huu una maana kubwa kwa timu nzima ya KWS,” alisema Simiyu.

Mbali na riadha, Lewa Safari Marathon imeendelea kuwa jukwaa muhimu la kuchangisha fedha kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori na maendeleo ya jamii. Tangu kuanzishwa kwake, mapato ya mashindano hayo yamechangia juhudi za uhifadhi, elimu, huduma za afya na miradi ya kuboresha maisha ya jamii katika eneo la Kaskazini mwa Kenya.

“Mbio hizi zimeonyesha kile kinachowezekana pale watu wanapoungana kwa lengo moja. Kufikia zaidi ya dola milioni 10 zilizochangwa ni mafanikio makubwa yanayoonyesha kujitolea kwa wakimbiaji, wadhamini, washirika na wafadhili kwa kipindi cha miaka 26,” alisema Rais na Mkurugenzi Mtendaji wa TUSK, Charley Mayhew.

Safaricom, ambayo imekuwa mdhamini mkuu wa mashindano hayo kwa miaka 26 mtawalia, ilitoa shilingi milioni 10 kusaidia kufanikisha makala ya  mwaka huu.

 

Taarifa yake Vincent Mogoi

Share This Article