Mrakibu wa Kaskazini Mashariki asema utulivu utarejeshwa Garissa

Tom Mathinji
2 Min Read
Mrakibu wa eneo la Kaskazini Mashariki ameapa kukabiliana vilivyo na wahalifu.

Mrakibu wa eneo la Kaskazini Mashariki John Otieno, amewaagiza maafisa wa usalama kukabiliana vilivyo na magenge ya wahalifu  mjini Garissa, kufuatia ongezeko la mashambulizi yanayohusishwa na vijana waliojihami kwa visu.

Agizo hilo linajiri huku mji wa Garissa ukighubikwa na ongezeko la visa vya uhalifu vinavyotekelezwa na vjana walio na umri wa kati ya miaka 11 na 20.

Mji huo umeshuhudia watu kushambuliwa kwa kudungwa visu, wizi, na mashambulizi wakati wa mchana, hatua ambayo imechangia biashara kufungwa mapema kutokana na hofu.

Kulingana na Mrakibu huyo, asasi za usalama zimeimarisha doria ili kurejesha utulivu na kuhakikisha wakazi wanaendeleza shughuli zao za kila siku.

“Mojawepo wa maswala ya kiusalama ambayo tunashughulikia ni kuibuka kwa magnge ya wahalifu wenye umri mdogo katika mji wa Garissa,” alisema Otieno.

Akizungumza kwenye mkutano wa usalama uliowaleta pamoja Kaunti Kamishna, Manaibu wa Kamishna wa Kaunti, Machifu na Manaibu wao, pamoja na Makamanda wa Polisi, Otieno alidokeza kuwa serikali imejitolea kudumisha utulivu, akisema wahalifu wote watachukuliwa hatua.

Aidha, alisema ongezeko hilo la visa vya utovu wa usalama ni tishio kwa usalama wa umma na shughuli za kiuchumi kwenye mji huo, huku akitoa wito wa hatua za pamoja baina ya mashirika ya usalama, viongozi wa kijamii na wazazi ili kutatua tatizo hilo.

Kamishna huyo pia alihimiza umma kugawana habari na mashirika ya usalama zitakazosaidia kutambua na kuwakamata wahusika.

Share This Article