Msemaji wa serikali Isaac Mwaura ameonya kuwa waandamanaji watakaozua vurugu wakati wa maandamano yaliyopangwa kufanywa Alhamisi wiki hii watakabiliwa vikali kisheria.
Vijana wa Gen Z Juni 25 wamepanga kuandaa maadhimisho ya miaka miwili tangu kufanyika kwa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.
Watu kadhaa walifariki na wengine wengi kujeruhiwa wakati wa maandamano hayo miaka miwili iliyopita.
“Ikiwa waandamanaji watazua vurugu kwa mujibu wa kifungu cha 82, polisi wanaruhusiwa kuchukua hatua kisheria bila athari zozote. Ikiwa watu watazua vurugu, polisi wana wajibu wa kuhakikisha wanadumisha sheria na utulivu,” alisema Mwaura wakati akiwahutubia wanahabari leo Jumatatu.
Wiki jana, Rais William Ruto alionya kuwa waandamanaji watakaopatikana wakizua vurugu na kujihusisha katika visa vya uporaji wakati wa maandamano hayo watakiona cha mtema kuni.
Ingawa alisema vijana wana uhuru wa kikatiba wa kufanya maandamano na kujieleza watakavyo, ni lazima wafanye hivyo kwa kuheshimu sheria za nchi.
Alionya dhidi ya kutatiza shughuli za kujenga nchi alizosema zitaendelea kama kawaida kote nchini kinyume cha matamanio ya waratibu wa maandamano hayo.