Madaktari 17 ni miongoni mwa watu zaidi ya 200 ambao wamefariki na ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Shirika la Afya Duniani WHO limesema wahudumu 75 wa afya wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo tangu DRC ilipotangaza chamko hilo Mei 25, 2026.
Aidha, Wizara ya Afya nchini humo imenakili visa 875 vya maambukizi ya Ebola, pamoja na vifo 202, ikidokeza kuwa watu 67 wamepona ugonjwa huo huku wagonjwa 379 wakilazwa katika sehemu za kuwatibu wagonjwa wa Ebola.
Wakati huo huo, wizara hiyo imesema kesi mpya 40 zimethibitishwa, ikiwemo vifo vinne katika mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini, na maeneo mawili zaidi ya afya, Fataki katika mkoa wa Ituri na Musienene mkoani Kivu Kaskazini yakiathiriwa na ugonjwa huo, na kufanya jumla ya maeneo ya afya yaliyoathiriwa kufikia 33 katika mikoa ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini.
Maafisa wa afya wanaamini aina ya virusi vya Ebola vinavyojulikana kama Bundibugyo vimekuwa vikisambaa kwa miezi kadhaa kabla ya serikali kutangaza rasmi chamko hilo, hali hiyo ikiwaacha madaktari, wauguzi na wafanyakazi wengine kwenye hatari ya kuambukizwa.
Uhaba mkubwa wa vifaa vya kimsingi vya kinga unashuhudiwa DRC, huku baadhi ya vituo vya afya vikikabiliwa na ukosefu wa glavu, barakoa pamoja na mahitaji mengine muhimu ya kudhibiti maambukizi.
Wanachama wa Umoja wa Afrika, wameahidi msaada wa dola bilioni moja kukabiliana na dharura Mashariki ya DRC pamoja na nchi jirani ya Uganda ambayo imethibitisha visa 19 vya maambukizi na vifo viwili.
Maafisa wa afya walionya kwamba chamko hilo bado halijafikia kilele chake.