Uchunguzi wa maiti za wanafunzi wa Utumishi Girls Academy waanza

Tom Mathinji
1 Min Read
Uchunguzi wa maiti za wanafunzi 16 wa Utumishi Girls Academy waanza.

Familia za wanafunzi 16 wa  Utumishi Girls Academy wamekusanyika katika hospitali ya kaunti ndogo ya Naivasha, huku uchunguzi wa maiti  ukitekelezwa na kusimamiwa na maafisa wakuu serikalini.

Uchunguzi huo wa maiti kubainisha utambulisho wao (DNA), ulianza leo Jumamosi huku wazazi waliojawa na majonzi wakisubiri kwa hamu nje ya kituo hicho cha afya.

Wanafunzi hao walifariki baada ya moto kuteketeza bweni lao usiku wa kuamkia Alhamisi, ambapo pia wanafunzi wengine zaidi ya 70 walijeruhiwa na wanaendelea kupokea matibabu.

Mnamo siku ya Ijumaa, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alitangaza kuvunjwa kwa bodi ya usimamizi wa shule hiyo, akidokeza kuwa uchunguzi unaendelea kubaini chanzo cha mkasa huo.

Aidha wanafunzi 8 wa shule hiyo wanazuiliwa na polisi kuhusiana na mkasa huo, huku shule hiyo ikifungwa kwa muda usiojulikana.

Mkasa huo umeibua tena wasiwasi kuhusu viwango vya usalama shuleni na kusababisha wito wa uchunguzi wa kina kufanywa na kuimarishwa kwa hatua za kulinda wanafunzi.

Share This Article