Wizara ya Afya ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imesema kuwa idadi ya watu walioambukizwa ugonjwa wa Ebola imefika 1,077.
Maafisa wa DRC wamesema ugonjwa huo sasa umeenea hadi katika maeneo 13 nchini humo, ikiwa ni pamoja na Ituri ambapo mlipuko huo uliripotiwa, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, huku mlipuko huo ukiendelea kuenea katika mikoa ya Mashariki ya Kati.
Hadi kufika sasa, ugonjwa wa Ebola umeathiri maeneo 13 ya afya katika mikoa ya mashariki ikiwemo Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambapo Ituri inaalia kuwa kiini cha mlipuko huo.
Tayari Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza mlipuko wa Ebola nchini DRC kuwa dharura ya afya ya umma, huku taifa jirani la Uganda likitangaza kufunga mpaka wake na DRC ili kudhibiti msambao wa ugonjwa huo.
Haya yanajiri huku WHO ikionya kuwa mzozo unaoendelea DRC unahujumu juhudi za kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini humo.
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema shirika hilo haliwezi kushughulikia janga hilo la Ebola huku mabomu yakilipuliwa.
Tedros anatarajiwa kuwasili nchini DRC leo Alhamisi, kuongoza juhudi za kukabili virusi hivyo.
Mlipuko huo wa Ebola ni wa 17 nchini DRC, huku uchunguzi wa kimaabara ukibaini kuwa ni wa aina ya virusi vya Bundibugyo, ambavyo ni aina nadra ya Ebola.