Wakenya watakiwa kuwa waangalifu kufuatia mlipuko wa Ebola nchi jirani

Martin Mwanje
1 Min Read

Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi amewataka Wakenya kuzingatia kanuni zinazotolewa na Wizara ya Afya kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani za Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC) na Uganda.  

Akizungumza huko Murang’a, Mudavadi amesema jinsi tu Wakenya walivyofanya wakati wa janga la COVID, wanapaswa kuwa waangalifu zaidi ili nchi hii isiathiriwe na ugonjwa wa Ebola.

Ameonya kuwa ingawa hakuna visa vya ugonjwa huo vimeripotiwa nchini kwa sasa, uzembe unaweza ukaiweka nchi hii pabaya na kutaka kanuni zote za afya kuzingatiwa.

“Tunahitaji kutii kanuni za afya zilizotusaidia kuokoa maisha wakati wa janga la COVID-19. Kwa sasa tunashuhudia aina hatari ya Ebola na katika nchi zetu jirani, ugonjwa huo tayari umesababisha vifo vingi,” alionya Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje.

“Inaonekana aina hii ya virusi haiwezi ikatibiwa wakati wowote hivi karibuni na hivyo tunapaswa kuwa waangalifu zaidi kuhusiana na usafi wetu na namna tunavyotangamana ili kujilinda.”

Umoja wa Afrika umeonya kuwa nchi 10 za bara la Afrika zimo katika hatari ya kukumbwa na maambukizi ya ugonjwa huo mbali na DRC na Uganda.

Share This Article