IEBC yatoa hakikisho uchaguzi mkuu 2027 utakuwa huru na wa haki

Tume hiyo imeonya wanaotoa madai ya wizi wa kura ikisema watachukuliwa hatua kali, na kuahidi uovu huo hautaruhusiwa kamwe kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Martin Mwanje
1 Min Read
Erastus Ethekon - Mwenyekiti wa IEBC

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imepuuzilia mbali madai kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 utakumbwa na wizi wa kura. 

Mwenyekiti wa tume hiyo Erastus Ethekon amewaonya wanasiasa wanaotoa madai kama hayo akisema watachukuliwa hatua kali za kisheria.

“IEBC itashirikiana na asasi husika ili hatua mwafaka ichukuliwe. Wakati umewadia kwa wanasiasa kukoma kudanganya umma kuwa uchaguzi utaibwa na badala yake waanze kukumbatia hatua zilizowekwa za maandalizi ya nchi ya kufanya uchaguzi mkuu wa mwaka 2027,” alisema Ethekon kwenye taarifa.

“Hebu kila mtu aheshimu uhuru wa kitaasisi kama ilivyoelezwa kwenye Katiba.”

Ethekon aliyasema hayo siku chache baada ya Naibu Gavana wa kaunti ya Kakamega Ayub Savula kudai kuwa utawala wa Kenya Kwanza utaiba kura za mwaka 2027.

Ni kauli ambazo zimeutia mashaka upande wa upinzani huku viongozi wake wakionya IEBC dhidi ya kujihusisha katika visa vyovyote vya wizi wa kura.

Awali, viongozi kadhaa wanaogemea utawala wa Kenya Kwanza pia wamenukuliwa wakitoa madai ya wizi wa kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

Uchaguzi mkuu nchini Kenya, hususan wa urais, hukumbwa na madai ya wizi wa kura miaka nenda miaka rudi, madai ambayo huishia na kupata suluhu katika Mahakama ya Juu.

 

Share This Article