Asilimia 70 ya waathiriwa wa dhuluma za kijinsia katika kaunti za eneo la Mlima Kenya ni wanaume. Hii ni kwa mujibu wa ripoti ya jopokazi lililobuniwa na Rais William Ruto kuchunguza visa vya dhuluma za kijinsia katika eneo hilo kati ya mwezi Juni mwaka jana na Aprili mwaka huu.
Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa zaidi ya visa 600 vimeripotiwa katika kaunti za Murang’a, Kiambu, Nyandarua, Laikipia na Nyeri ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja, huku wengi wa waathiriwa wakiwa wanaume wenye umri wa zaidi ya miaka 40.
Akizungumza na wanahabari katika warsha ya siku moja mjini Nyeri, Katibu katika Wizara ya Jinsia Anne Wang’ombe alitaja ukosefu wa ajira, matumizi ya pombe haramu, dawa za kulevya pamoja na msongo wa mawazo kuwa baadhi ya vyanzo vikuu vya dhuluma za kijinsia.
Wang’ombe pia alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali katika kukabiliana na tatizo hilo. Aidha, alitangaza kubuniwa kwa jopo litakalowajumuisha wadau kutoka kaunti tano za eneo la Kati mwa Kenya ili kutathmini mbinu za kukabili dhuluma za kijinsia na kuwasilisha ripoti ndani ya kipindi cha siku tisini.
Wakati huo huo, serikali imesema itazichukulia hatua shule zinazowalazimu wanafunzi kufika mapema kabla ya muda uliowekwa rasmi, kufunga vilabu vinavyouza pombe haramu, pamoja na kuwachukulia hatua za kisheria washukiwa wa dhuluma za kijinsia kama sehemu ya juhudi za kukabiliana na tatizo hilo.
Kwa upande wake, Kamishna wa eneo la Kati mwa Kenya Joshua Nkanatha ameahidi ushirikiano wa vyombo vya usalama katika kuhakikisha visa hivyo vinadhibitiwa haraka iwezekanavyo.
Warsha hiyo imeandaliwa kufuatia eneo la Kati mwa Kenya kuripotiwa kuathirika zaidi na visa vya dhuluma za kijinsia pamoja na ukeketaji ikilinganishwa na maeneo mengine nchini.
Taarifa ya William Khaemba