Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC), imewakamata washukiwa 11 wanaodaiwa kufuja fedha katika Hazina ya Maendeleo ya Maeneo Bunge (NG-CDF) ya eneo bunge la Eldama Ravine.
Washukiwa hao wanajumuisha wanachama wa kamati ya NG-CDF na maafisa wa kaunti ndogo ambao wanadaiwa kupora fedha ambazo zilikuwa zimetengewa eneo bunge la Eldama Ravine.
EACC ilipokea malalamishi kwamba, kati ya mwaka wa fedha wa 2018/2019 na ule wa 2020/2021, hazina ya NG-CDF ya Eldama Ravine ilipoteza takriban shilingi milioni 85, na kusababisha miradi ya maendeleo kukosa kutekelezwa katika eneo hilo.
Kulingana na ripoti ya EACC, eneo bunge hilo lilipokea shilingi 369,052,479 katika mwaka wa fedha wa 2018/2019, 2019/2020na 2020/2021 kutoka kwa bodi ya NG-CDF.
Baada ya kukamilisha uchunguzi wake, EACC iliwasilisha ripoti kwa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ambaye aliidhinisha mashtaka dhidi ya washukiwa hao.
Washukiwa hao ni pamoja na Geofrey Koech (Meneja wa Hazina hiyo), Solomon Mwaura Kiratu (Msahibu wa zamani wa kaunti ndogo ya Koibatek), Joseph Kibor Aiyabei (Mwenyekiti wa kamati ya NG-CDF), Ann Mwihaki Mwangi, Dickson Kiplagat Chelimo na Peter Kiptanui.
Wengine ni Evans Kiprono Keter (Mhasibu wa Clerk, NG-CDF Eldama Ravine), Stephen Kipyegon Bundotich (Afisa wa ICT wa NG-CDF Eldama Ravine) Evans Kipngetich Kiptoo, Musa Kiplagat Ngetich, Walter Zali Avihama, Kipruto Yegon, na Anthony Cherogony Toroitich.
Washukiwa hao watafunguliwa mashtaka ya utumizi mbaya wa mamlaka, kupata mali kwa njia ya udanganyifu, na utepetevu wa majukumu miongoni mwa mengine.