Rais William Ruto ameiagiza Wizara ya Elimu kukumbatia mfumo wa dijitali, kuwezesha upatikanaji wa maelezo sahihi ili kuhakikisha ufanisi wa mipango na uwajibikaji.
“Nimeagiza Wizara ya Elimu kuweka maelezo ya wanafunzi kwa mfumo wa dijitali katika muda wa miezi miwili ijayo, ili kuimarisha uwajibikaji,” alisema Rais Ruto.
Kiongozi huyo alisema mfumo wa dijitali utafanikisha kuziba mianya ambayo imesababisha serikali kupoteza mabillioni ya pesa kupitia wanafunzi na shule hewa.
Kulingana na Rais Ruto, ripoti ya ukaguzi wa wanafunzi imeashiria kuwepo wanafunzi hewa 87,000 katika shule za upili, wanafunzi hewa 800,000 katika shule za msingi na shule hewa 200 kote nchini.
“Serikali imekuwa ikilipa shilingi bilioni 1.2 kila mwaka kwa wanafunzi ambao hawapo. Tunawauliza baadhi ya walimu wakuu maswali magumu, na baadhi ya viongozi katika wizara ya elimu katika viwango vya kaunti,” alisema Rais Ruto.
Rais aliyasema hayo Alhamisi wakati wa ufugunguzi wa kongamano la pili la kitaifa kuhusu elimu, lililoandaliwa mjini Naivasha, kaunti ya Nakuru.