Ujenzi wa bwawa la Mwache katika kaunti ya Kwale, unatarajiwa kukamilika mwaka huu, kabla ya muda uliowekwa, hayo ni kulingana na mwanakandarasi wa mradi huo.
Hata hivyo kamati ya Bunge la Taifa kuhusu Maji, Unyunyizaji Mashamba Maji na Uchumi wa Majini, imeonya kuwa mradi huo wa kitita cha shilingi bilioni 25.6 ambao umekamilika asilimia 83, huenda ukakumbwa na ucheleweshaji kutokana na ukosefu wa ufadhili wa ujenzi wa mabomba ya usambazaji maji.
Kamati hiyo ilitoa onyo hilo wakati wa ziara ya kukagua ujenzi wa bwawa hilo, baada ya mkandarasi ambayo ni kampuni ya Sinohydro, kupunguza kazi ya ujenzi kutokana na ucheleweshwaji wa malipo.
Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni mbunge wa Marakwet Mashariki Kangogo Bowen, alisema mradi huo ulio katika eneo bunge la Kinango, amepiga hatua kubwa, lakini ukosefu wa fedha umedumaza kasi ya utendakazi.
“Tumeridhishwa na hatua zilizopigwa kwenye mradi huu, ambao ujenzi wake umefika hatua 83. Hata hivyo kasi ya ujenzi huo umepungua kutokana na ucheleweshaji wa malipo,” alisema Bowen.
Bowen alitoa wito kwa Wizara Maji, Unyunyizaji mashamba maji na Uchumi wa Majini, kuharakisha uwekaji wa miundombinu ya usambazaji maji, akiongeza kuwa wakazi wa Kwale wanapaswa kupewa kipaumbele kabla ya maji hayo kusambazwa kwa kaunti jirani ya Mombasa.
Kulingana na Bowen, mwanakandarasi huyo anadai kulipwa shilingi bilioni 1.9, akidokeza kuwa kamati yake itaishinikiza wizara ya fedha kutoa fedha ili kufanikisha kukamilika kwa ujenzi huo kwa wakati.