Waziri wa Nishati na Petroli Opiyo Wandayi, amethibitisha kuwa Kenya ina mafuta ya kutosha, na kuondoa hofu kuhusu uhaba wa bidhaa hiyo muhimu hapa nchini.
Kulingana na waziri huyo, uhaba wa mafuta ya petroli ambao ulioripotiwa kwenye vituo kadhaa vya kuuza mafuta kote nchini, umesababishwa na hitilafu ya kimitambo.
Hata hivyo kupitia kwa taarifa, Wandayi amewahakikishia Wakenya hitilafu hiyo inashughulikiwa, na kwamba usambazaji wa kawaida wa mafuta ya petroli utarejelewa.
Wandayi alisema uhaba huo wa muda umeathiri vituo vichache pekee vya kuuza mafuta hayo, kutokana na changamoto kwenye shughuli za kusambaza mafuta.
Hakikisho hilo linafuatia madai ya uhaba wa mafuta katika vituo kadhaa vya mafuta jijini Nairobi, ambao ulisababisha wasiwasi miongoni mwa waendeshaji magari na wafanya biashara kuhusiana na changamoto ya uhaba huo.
Wizara hiyo inasisitiza kwamba nchi hii ina mafuta ya kutosha huku ikitoa wito kwa wananchi kutokuwa na hofu. Wandayi alisisitiza kujitolea kwa serikali kuhakikisha kuna kawi ya kutosha kote nchini na kwamba mafuta ya petroli yatasambazwa bila kukatizwa.