Meli iliyokumbwa na mlipuko wa Hantavirus kutia nanga Uhispania

Wafanyakazi wawili, akiwemo daktari wa meli, wanahitaji matibabu ya haraka na wanasubiri kuhamishwa.

KBC Digital News
2 Min Read
Meli iliyokumbwa na ugonjwa wa Hantavirus kutua katika visiwa vya Canary.

Meli ya kitalii ya Uholanzi, MV Hondius, ambayo imekumbwa na mlipuko wa Hantavirus, inatarajiwa kuelekea Visiwa vya Canary nchini Hispania, kulingana na taarifa ya serikali.

Wizara ya afya ya nchini humo imesema maafisa wanachunguza abiria  wanaohitaji kuhamishwa haraka kutoka Cape Verde, ambako meli hiyo ilikuwa imetia nanga.

Abiria waliobaki wataendelea na safari kuelekea visiwa vya Canary, ambapo wanatarajiwa kufika ndani ya siku tatu hadi nne, ingawa bandari kamili ya kuwasili bado haijaamuliwa. Kampuni ya safari, Oceanwide Expeditions, imesema mpango ni kuelekea “Gran Canaria au Tenerife”.

Watu watatu waliokuwa ndani ya meli hiyo wamefariki tangu ilipoondoka Argentina karibu mwezi mmoja uliopita kwa safari yake ya kuvuka Bahari ya Atlantiki.

Wafanyakazi wawili, akiwemo daktari wa meli, wanahitaji matibabu ya haraka na wanasubiri kuhamishwa. Mtu mwingine anayehusishwa na raia wa Ujerumani aliyefariki pia anatarajiwa kuhamishwa.

Katika taarifa yake, wizara ilisema daktari huyo, ambaye yuko katika hali mbaya, anatarajiwa kupelekwa katika Visiwa vya Canary Jumanne kwa ndege ya hospitali.

Iliongeza kuwa WHO imeeleza kuwa Cape Verde “haiwezi kutekeleza operesheni hiyo”.

“Visiwa vya Canary ndivyo vilivyo karibu zaidi vyenye uwezo unaohitajika. Hispania ina wajibu wa kimaadili na kisheria kusaidia watu hawa, miongoni mwao wakiwemo raia kadhaa wa Hispania,” ilisema taarifa hiyo.

Taarifa na BBC

Share This Article