Mhubiri tata wa nchini Kenya Paul Mackenzie, aliwahimiza wafuasi wake kususia chakula, akisema ilikuwa ni dhambi kula chakula.
Hayo yaliibuka mahakamani wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya mauaji ya Shakahola iliyoanza Jumatatu katika Mahakama Kuu ya Mombasa.
Mbele ya Jaji Diana Kavedza, Lucas Owino Ogok, ambaye ameshtakiwa kwenye kesi hiyo,alipokuwa akihojiwa na Naibu Kiongozi wa Mashtaka ya Umma Jami Yamina, alikiri kuwa Mackenzie aliwalazimisha wafuasi wake kususia chakula, hatua iliyosababisha vifo vya zaidi ya watu 400.
Owino alifahamisha mahakama kuwa alikumbatia imani kuwa elimu ilikuwa ni maovu, kwa sababu iliwafanya watu kuwa na mafikira tofauti.
Mshitakiwa mwingine kwenye kesi hiyo Steven Sanga, almaarufu Steve wa Mtwapa, alielezea jinsi alivyosafiri kutoka Mtwapa kuelekea Shakahola kufuatia changamoto ya ukosefu wa fedha wakati wa janga la Covid-19.
Mark Kiongera Kiarie, ambaye pia ni mshtakiwa kwenye kesi hiyo, alifahamisha mahakama kuwa alishiriki mikutano ambapo wakazi walikiri mipango ya kususia chakula hadi kufa, na hata alisaidia kuzika mwili bila jeneza.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa leo Jumanne, huku watu kadhaa wakitarajiwa kutoa ushahidi.