Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeelezea kujitolea kwake kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Usalama wa Taifa, washirika wa maendeleo na wadau wengine kuhakikisha Uchaguzi Mkuu unakuwa wa amani, huru, na wenye uwazi.
Akizungumza wakati wa mkutano wa mashauriano na Wizara ya Usalama wa Taifa, mwenyekiti wa IEBC Erastus Ethekon, alisisitiza kuwa ufanisi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027, utategemea pakubwa na jinsi taasisi husika zitashirikiana wakati wa uchaguzi huo.
“Uchaguzi sio jukumu la taasisi moja. Ufanisi katika Uchaguzi unategemea ushirikiano dhabiti, mashauriano ya kina, na uungwaji mkono miongoni mwa taasisi zilizojukumiwa kulinda demokrasia, amani, usalama na uzingatiaji sheria,” alisema Ethekon.
Mwenyekiti huyo aliishukuru Wizara ya Usalama wa Taifa kutokana na usaidizi wake wakati wa zoezi usajili endelevu wa wapiga kura uliokamilika Alhamisi Mei 14, 2026.
Kwa upande wake, Waziri wa Usalama wa Taifa Kipchumba Murkomen, aliihakikishia IEBC ushirikiano thabiti kuhakikisha ufanisi kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2027.
Mkutano huo ulioandaliwa Ijumaa Mei 15, 2026, uliangazia ushirikiano hususan katika utoaji wa vitambulisho vya taifa, usalama wakati wa uchaguzi na utatuaji wa mizozo.