Chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka kimejitenga na matamshi yaliyotolewa na ,wanachama wake Farah Maalim.
Maalim ambaye ni mbunge wa eneo la Dadaab na naibu kiongozi wa chama cha Wiper alinakiliwa kwenye video akisema kwamba angekuwa kiongozi wa nchi angechukua hatua ya kuwatoa uhai vijana wa kizazi cha Z ambao wamekuwa wakiandamana.
Matamshi yake yamezua lalama kote mitandaoni huku wakenya wakitaka kwamba aondolewe kwenye wadhifa wake.
Katika taarifa kwa wanahabari leo, chama hicho cha Wiper kilitangaza kwamba hakikubaliani kwa vyovyote na matamshi ya Farah kwani yanakwenda kinyume na kanuni za chama.
Adhabu ambayo chama cha Wiper kimeamua kutoa dhidi ya mbunge huyo ni kumwondoa kwenye kamati zote za bunge na hata kwenye baraza la spika.
Wanachama wengine chama hicho pia wako matatani kwa kukiuka msimamo wa chama mara kadhaa, ukiukaji wa hivi punde zaidi ukiwa kuhusu mswada wa fedha.
Mwakilishi wa kaunti ya Kisii bungeni Doris Donya Toto alikosa kupiga kura wakati wa kupitishwa kwa mswada wa fedha huku mbunge mteule Abubakar Ahmed na mbunge wa Taveta John Okano Bwire wakiuunga mkono.
Wanne hao walikuwa wameitwa kuhudhuria kikao cha baraza kuu la chama cha Wiper leo ila hawakujitokeza na sasa kesi zao zimewasilishwa kwa kamati ya nidhamu ya chama hicho.