Seneta wa kaunti ya Nairobi Edwin Sifuna, alikuwa miongoni mwa viongozi wa Bara Afrika waliozuiwa kuingia Angola na serikali ya nchi hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa X leo Alhamisi, Sifuna alisema aliwasili salama Addis Ababa baada ya kutimuliwa Angola, huku akishukuru ubalozi wa Kenya kwa kufanikisha kuondoka kwake nchini humo.
“Nimewasili salama Addis baada ya kutimuliwa Angola. Nashukuru ubalozi wa Kenya nchini Angola ukiongozwa na balozi Joyce Mmaitsi.,” alisema Sifuna kupitia kurasa wa X.
Sifuna alipachika barua ya mwaliko wa mkutano huo kwenye ukurasa wake wa X, kuthibitisha alikuwa amealikwa na Rais wa UNITA, Adalberto Costa nchini Angola.
Vyanzo vya habari vinasema kuwa takriban viongozi 40 walizuiwa kuingia Angola na mamlaka ya nchi hiyo.
Baadhi ya wale waliozuiliwa ni pamoja na Rais wa zamani wa Botswana Ian Khama, Waziri Mkuu wa zamani wa Lesotho, mwenyekiti wa chama kikuu cha Upinzani Tanzania, CHADEMA, Tundu Lissu, Kiongozi wa upinzani Uganda, Robert Kyagulanyi (Bbobi Wine) na mwenyekiti wa Chama cha upinzani cha ACT nchini Tanzania, Othman Masoud Othman.
Viongozi hao waliwasili Angola kushiriki mazungumzo ya siku nne kuanzia Machi 13 hadi 16, kuhusu Demokrasia Afrika, yaliyoandaliwa na wakfu wa The Brenthurst.
Angola haijasema lolote kuhusu swala hilo.