Watu 14 wafariki kwenye ajali ya barabara Migaa

Dismas Otuke
1 Min Read

Watu 14 wameuawa mapema leo Ijumaa kwenye ajali ya barabarani iliyotokea katika eneo la Migaa, Molo, kwenye barabara kuu ya Nakuru-Eldoret majira ya saa tisa alfajiri.

Ajali hiyo ilihusisha gari la Kitale Shuttle la abiria 11 lililokuwa likielekea Nairobi kutoka Kitale, na trela la kubeba mizigo ambalo pia lilikuwa njiani kwenda Nairobi.

Kulingana na ripoti ya Naibu Kamanda wa Molo Timon Odingo, dereva wa lori hilo la kubeba shehena ya kontena alipoteza mwelekeo na kugonga gari la abiria huku abiria wote 12 kwenye matatu hiyo wakifariki papo hapo.

Watu wengine wawili waliokuwa kwenye lori akiwemo dereva pia waliangamia.

Waliofariki ni pamoja na wanaume tisa, wanawake wanne, na mtoto mmoja.

Inaaminika trela hiyo iligonga matatu hiyo na kuiburura kwa muda na kusababisha watu wote waliokuwa kwenye magari hayo mawili kukwama ndani.

Mili ya walioaga dunia imepelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti.

Shirika la Msalaba Mwekundu limefungua kituo cha kutoa ushauri nasaha kwa familia za waliofariki.

Eneo la Migaa linaaminika kuwa hatari na ajali nyingi hutokea hapo mara kwa mara.

Website |  + posts
Share This Article