Mama Taifa Rachel Ruto Leo Jumatano amezindua rasmi mpango wa kitaifa wa bustani za chakula nyumbani, ambazo alisema zitahakikisha utoshelevu wa chakula zilizo na virutubisho katika jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo ulioandaliwa katika eneo la Koibatek, kaunti ya Baringo, Mama Taifa alisema Kupitia bustani hizo, kina mama wataimarika kiuchumi nà kutokomeza utapiamlo miongoni mwa watoto.
” Kila mama hufurahia anapoona jamii yake inapata lishe bora,” alisema Mama Taifa.
Alisema Kupitia mpango wa bustani za chakula nyumbani, wanafunzi wengi wamepata motisha ya kuendelea na masomo, kutokana na afya yao nzuri na hakikisho kwamba Kuna chakula nyumbani.
“Huwezi mfundisha mtoto aliye na njaa.Utapiamlo na njaa ni changamoto kwa masomo, maendeleo na ufanisi,” aliongeza Mama Taifa.
Alitoa wito kwa kila familia kuhakikisha zina bustani za chakula, ili kufanikisha ajenda ya serikali ya Rais William Ruto ya kuwa na utoshelevu wa chakula hapa nchini.

Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu katika wizara ya kilimo Dkt. Kipronoh Ronoh, alisema bustani za chakula nyumbani ni muhimu sana Kwa upatikanaji wa chakula mijini na maeneo kame.
Dkt. Ronoh alisema mpango huo unaoongozwa na Mama Taifa, unalenga kuwa na bustani za chakula milioni mbili, katika familia na shule milioni moja kote nchini.
“Mpango huu unapiga jeki mfumo wa kiuchumi wa Bottom-Up wa kuimarisha uzalishaji chakula na kuboresha lishe,” alisema Dkt. Ronoh.
Miongoni mwa wale waliohudhuria uzinduzi huo ni pamoja na Waziri wa Mazingira Dkt. Deborah Barasa.