Odinga aambia Gen Z kwamba amepata ujumbe wao

Marion Bosire
2 Min Read

Kiongozi wa mrengo wa upinzani Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga ameambia vijana wa “Gen Z” kwamba amepata ujumbe wao kuhusiana na maridhiano.

Odinga ambaye pia ni kiongozi wa chama cha ODM alichapisha picha akiwa pamoja na viongozi wa umri mdogo waliochaguliwa na chama cha ODM kwenye mitandao ya kijamii kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii.

Aliandika, “Nimeambiwa na hawa viongozi kwamba mumesema hamtaki handshake. Ujumbe umefika.”

Haya yanajiri kufuatia hatua ya Raila ya kujitolea kushiriki mazungumzo na serikali kujaribu kutatua masuala yaliyoibuliwa na vijana wa Gen Z wakati wa maandamano ya kupinga mswada wa fedha.

Raila alitangaza hayo jana muda mfupi baada ya kushuhudia kutiwa saini kwa mswada wa marekebisho ya tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC na Rais William Ruto jana.

Vijana wa Gen Z walitumia mitandao ya kijamii kupaaza sauti zao kulalamikia hatua ya Odinga ambayo waliichukulia kuwa ujio wa maridhiano kati yake na serikali.

Awali vijana hao kupitia mitandao ya kijamii walimsihi Odinga asiingilie maandamano yao awape fursa kwani yeye alishatekeleza jukumu lake awali na sasa ni wakati wao.

Viongozi waliofanya mazungumzo na Raila Odinga leo kwenye afisi yake ni pamoja na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Seneta mteule Crystal Asige, mbunge mteule Irene Mayaka na seneta wa kaunti ya Migori Eddy Oketch.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *