Makachero wa eneo la Kilimani, kaunti ya Nairobi wamewakamata watu watatu wanaoshukiwa kuvunja nyumba na kuiba vitu kadhaa katika eneo la Westlands, kaunti ya Nairobi wiki tatu zilizopita.
Wakati wa tukio hilo, bidhaa kadhaa za elektroniki, dola 24,500 za Marekani na bidhaa zingine ziliibwa.
Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI inasema imewakamata Lenah Khamatioli mwenye umri wa miaka 28, Ian Kavaya (28) na Peninah Mutola (32) kutoka maficho yao katika mtaa wa Kawangware kwa kushukiwa kutekeleza wizi huo.
Wizi huo ulifanywa Septemba 24 mwaka huu kwenye nyumba inayomilikiwa na raia wa Sudan Kusini inayopatikana kwenye barabara ya Rahpta mtaani Westlands.
DCI inasema raia huyo aliwasili nyumbani na kupata yaya wake akiwa hayuko na dola 24,500 za Marekani na simu aina ya iPhone 15 miongoni mwa bidhaa zingine zikiwa zimeporwa.
Wakati wakikamatwa, washukiwa walikuwa na bidhaa kadhaa mpya ikiwa ni pamoja na pikipiki aina ya Boxer yenye nambari ya usajili KMGN 840N, runinga yenye ukubwa wa inchi 55 aina ya Vitron, maikrowevu aina ya Hanmac na simu tatu mpya aina ya Samsung A50. Bidhaa zote hizo zilinaswa.
Isitoshe, washukiwa walipatikana na makubaliano ya ununuzi wa kipande cha ardhi chenye thamani ya shilingi 423,000 katika eneo la Kapkangani, kaunti ya Nandi.
Washukiwa kwa sasa wanazuiliwa huku uchunguzi wa kubaini waliko washukiwa wengine wa wizi huo na bidhaa zilizoibwa ukiendelea.