Washukiwa wanne wamekamatwa katika eneo la viwandani Jijini Nairobi, kwa madai ya uharibifu na wizi wa miundombinu ya reli.
Maafisa wa Polisi waliwakamata washukiwa hao baada ya kupokea habari kutoka kwa wananchi, ambapo walifumaniwa wakikata vyuma vya reli katika eneo la Fuji, wakitumia gesi.
“Polisi walifika katika eneo hilo na kuwapata washukiwa hao wakiwa wamejificha kwenye kichaka kilicho karibu, na kuwakamata kabla hawajatoroka,” ilisema Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwenye ukurasa wake wa X.
Baada ya kufanya upekuzi, maafisa hao walipata mitungi miwili ya gesi, inayoshukiwa ililenga kufanikisha ukataji wa vyuma vya reli, huku uchunguzi wa awali ukibainisha washukiwa hao tayari walikuwa wamekata na kuiba vyuma vya urefu wa kati ya mita tatu na tano.
DCI ilisema juhudu za kupata vyuma vingine vya reli vilivyokuwa vimekatwa, zinaendelea.
Wasshukiwa hao wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi, wakisubiri kufikishwa kotini.