Kamati ya Kudumu ya Seneti kuhusu Elimu imemwelekeza Inspekta Jenerali wa Polisi, Douglas Kanja, kutoa hati ya kumkamata Gavana wa kaunti ya Tharaka Nithi, Muthomi Njuki.
Wito huo umechochewa na hatua ya Gavana huyo ya kukosa mara kwa mara kuhudhuria vikao vya kamati kila anapoitwa.
Kamati hiyo inataka Gavana Njuki afikishwe mbele yake tarehe 17 Novemba 2026 ili kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mipango ya Elimu ya Chekechea, ECDE, pamoja na mipango ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ya Kaunti ya Tharaka Nithi.
Kwa mujibu wa kamati hiyo, gavana huyo ameshindwa kufika licha ya mialiko na miito kadhaa iliyotolewa tangu mwezi Machi. Kamati pia ilimtoza faini ya Sh500,000 mnamo Agosti 4 kwa kushindwa kuhudhuria miito ya awali.
Faini hiyo iliwasilishwa mnamo Agosti 19, lakini hakufika mbele ya kamati wala kulipa adhabu hiyo.
Wito wa hivi karibuni ulimtaka Gavana Njuki kufika mbele ya kamati leo tarehe 1 Oktoba mwaka 2026 na kuwasilisha taarifa kwa maandishi kuhusu mipango ya elimu ya kaunti. Hata hivyo, hakuhudhuria tena.
Kamati imesema uwepo wa gavana ni muhimu ili kutoa ufafanuzi kuhusu utekelezaji wa majukumu ya elimu yaliyogatuliwa na changamoto zinazoathiri utoaji huduma katika kaunti hiyo.
Anatarajiwa kufika mbele ya kamati tarehe 17 Novemba saa 3 asubuhi.