Wapelelezi kutoka Idara ya Upelelezi wa Jinai, DCI huko West Pokot wamewakamata washukiwa 9 kuhusiana na ubadhirifu wa shilingi milioni 260 za chama cha akiba na mikopo.
Tisa hao walifikishwa katika mahakama ya Kapenguria ili kujibu mashtaka baada ya chama hicho kuwasilisha malalamiko kwa DCI huko West Pokot.
Katika malalamiko yake, chama hicho kilielezea mashaka juu ya ulaghai na ubadhirifu wa fedha unaohusisha baadhi ya maafisa wake wa sasa na wa zamani.
Matokeo ya awali yalifichua sakata ya ulaghai unaodaiwa wa fedha huku washukiwa wakikula njama ya kukarabati rekodi za fedha, kuhamisha kinyume cha sheria fedha za wanachama, uwezeshaji wa usambazaji usioidhinisha wa mikopo na kushindwa kuwajibikia kiasi kikubwa cha fedha walizopewa jukumu la kuzitunza katika utendaji kazi wao.
Tisa walioshtakiwa ni Fredrick Kaptui Plimo ambaye ni Spika wa sasa wa bunge la kaunti ya West Pokot, Linus Lokira ambaye ni Afisa Mkuu Mtendaji wa chama hicho, Paul Loktari Ywapamoi ambaye ni Mwakilishi Wadi ya Kodich na Leonard Pchakasan Domoita ambaye ni Meneja wa zamani wa Fedha.
Wengine ni Nicholas Toroitich Arusha ambaye ni Mhasibu wa zamani, Andrew Poriot Lorena ambaye ni Meneja wa zamani wa ICT, Susan Chesang, Florence Chemotwo na Francis Atodosia.
Washukiwa hao walikana mashtaka na kuachiliwa kwa dhamana ya kati ya shilingi milioni 10 na 11 na mdhamini wa kiasi kama hicho, au dhamana ya shilingi milioni 5 na milioni 6 pesa taslimu.
Kesi hiyo itatajwa Novemba 30.