Washukiwa 8 wamekamatwa baada ya kuhusishwa na sakata ya kuchanganya mbolea na vitu vingine na kisha kupakia upya.
Maafisa wa usalama waliwakamata Washukiwa hao katika Kijiji cha Ejinja, kaunti ndogo ya Rurambi kaunti ya Kakamega.
Washukiwa hao ni pamoja na Napoline Murende Wakukha, Isaya Chepkose Marende, Brivin Yeswa, Milkzadek Meja Nandwa, Martin Shilabula, Strola Deptica, Pascal Wathika Omusikoyo, na Jesca Bulimo.
Mbolea iliyonaswa inajumuisha ile ya serikali ya bei nafuu aina ya UREA TOSHA, OCP Africa TSP, DAP, YARA na CALCIGROW.
Aidha Magari mawili, mashine 3 za kushona na kemikali zilizoshukiwa kutumiwa kubadili rangi ya mbolea pia vilinaswa.
Kulingana na Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCI, washukiwa hao waliwashawishi wakulima kuchukua mbolea inayotolewa na serikali kwa niaba yao kabla ya kuichanganya na vitu vingine, kuipakia upya na kuiuza kwa bei za kawaida.
Maafisa wa serikali wanashuku ushirikiano wa washukiwa hao na baadhi ya wafanyakazi katika mabohari ya halmashauri ya nafaka na mazao NCPB huko Voi na Webuye.
Washukiwa hao watasalia korokoroni huku uchunguzi ukiendelea.