Washukiwa 2 wa ufujaji fedha za msaada wa masomo West Pokot wakamatwa

Martin Mwanje
2 Min Read

Tume ya Maadili a Kupambana na Ufisadi, EACC leo Jumatatu imewakamata washukiwa wawili kati ya wanne kuhusiana na ufujaji wa fedha za umma ambazo thamani yake ni milioni 296 katika kaunti ya West Pokot. 

EACC inasema fedha hizo ziliibwa kati ya kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018 na 2021/2022.

Washukiwa hao, Mary Ngoriakes ambaye ni afisa wa zamani wa elimu na Mathew Arusio ambaye mkurugenzi wa zamani wa msaada wa masomo, sasa watafikishwa katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi wakikabiliwa na mashtaka ya ufisadi.

“Washukiwa kwa sasa wapo katika Ofisi za EACC Kanda ya North Rift mjini Eldoret na baadaye watazuiliwa katika kituo cha polisi cha Eldoret Central wakisubiri kufikishwa katika Mahakama ya Kupambana na Ufisadi ya Eldoret kesho Jumanne, Septemba 24, 2024, saa 3 asubuhi,” amesema Eric Ngumbi, Msemaji wa EACC katika taarifa.

Tume hiyo ilianzisha uchunguzi baada kupokea malalamiko kwamba maafisa waandamizi katika serikali ya kaunti ya West Pokot walikula njama ya kuilaghai serikali hiyo shilingi milioni 212 kutoka kwenye Hazina ya Msaada wa Masomo, Elimu na Miundombinu ya kaunti hiyo.

Hata hivyo, EACC kupitia uchunguzi wake ilibaini kuwa fedha zilizoporwa ni shilingi milioni 296.

Washukiwa wawili, Simon Kodomuk na Francil Tikol ambao wapo mafichoni, wametakiwa kujisailimisha kwa ofisi za EACC za Kanda ya North Rift mjini Eldoret kesho Jumanne ili kufunguliwa mashtaka.

 

Website |  + posts
Share This Article