Wawakilishi wadi wa kaunti ya Machakos, wametangaza kuwa watarejelea vikao vya kamati za bunge hilo Ijumaa Mei,23,2025, hatua inayoonekana kukiuka agizo la Spika wa bunge hilo la kufutilia mbali vikao hivyo kwa muda usiojulikana.
Akiwatubia wanahabari siku ya Alhamisi, kiongozi wa wengi katika bunge la kaunti ya Machakos Nicholas Nzioka, alisema baada ya kufanyia marekebisho sehemu ya 161 ya kanuni za bunge inayompa karani wa bunge na wala sio Spika mamlaka ya kuandaa mikutano ya kamati za bunge, wawakilishi wadi hao waliazimia kurejelea vikao vya kamati za bunge hilo.
“Ilani kuhusu mkutano wa kamati unapaswa kutoka kwa karani wa bunge na wala sio kwa Spika. Hatua ya Spika ya kufutilia mbali vikao vya kamati za bunge, inakiuka mamlaka yake,” alisema Nzioka.
Alisisitiza kuwa wawakilishi wadi wote 59, watarejea bungeni kushughulikia maswala ya kamati ambayo hayawezi ahirishwa.
Spika wa bunge la kaunti ya Machakos Ann Kiusya alifutilia mbali shughuli zote za bunge hilo mwezi jana baada ya ghasia kuzuka zilizosababisha majeraha kwa wawakilishi wadi wawili.
Bunge la Senate limemwagiza Spika Kiusya, Wawakilishi Wadi na Karani wa bunge hilo kufika mbele yake Jumanne ijayo kutafuta suluhisho la changamoto linaloghubika bunge hilo.