Wangamati awasili EACC

Yeye na washirika wake wanahusishwa na kampuni mbali mbali zinazoaminika kutumiwa kufuja pesa za umma.

Marion Bosire
2 Min Read

Aliyekuwa Gavana wa kaunti ya Bungoma Wycliffe Wangamati amewasili katika afisi wa tume ya maadili na kukabiliana na ufisadi nchini EACC kama alivyoagizwa.

Wangamati ni mmoja wa maafisa waliotajwa na EACC Ijumaa Agosti 29, 2025 na anachunguzwa kwa madai ya ufujaji wa pesa za umma.

Gavana huyo wa zamani na washirika wake wanadaiwa kuhusika na kampuni mbali mbali za ujenzi na za uwasilishaji wa bidhaa na huduma.

Washirika wake waliotajwa na EACC ni pamoja na Michael Simiyu Wangamati, Nicholas Wangamati, Edward Barasa Wangamati, Edward Maaya Makhanu, Sandra Soita Nasambu na Wafula Wakoli Chesititi.

Wengine ni Bramwel Mukwe Wafula, Juma Swaleh Juma, Jimmy Wekesa Barasa, Christopher Masika Makokha na Joseph Wanyonyi Khaemba.

Wote hao walihitajika kufika kwenye afisi za EACC katika jumba la Integrity jijini Nairobi leo Jumatatu Septemba 1, 2025 saa mbili asubuhi.

Gavana wa kaunti ya Bomet Hillary Barchok naye alipatiwa mwaliko sawia na EACC na anatarajiwa pia kufika huko. Anachunguzwa kwa kile kinachotajwa kuwa mgongano wa maslahi.

Ametajwa katika kesi hiyo pamoja na Evans Kipkoech Korir ambaye ni mkurugenzi katika kampuni ya ujenzi ya Chemasus.

EACC ilitangaza kwamba iliamua kuchukua hatua ya kuchunguza watu hao kabla yao kufikishwa mahakamani kufuatia idhini kutoka kwa afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma DPP.

Share This Article