Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, ameshutumu dhidi ya mkondo wa siasa za kikabila na migawanyiko, akionya kuwa huenda zikasababisha athari mbaya hapa nchini.
Akizungumza leo Jumamosi wakati wa mkutano uwezeshaji kiuchumi katika maeneo bunge ya Likoni na Jomvu, Wetang’ula aliwahimiza Wakenya kuwakataa viongozi wanaopigia debe siasa za migawanyiko, akiwataka kuzingatia umoja, utoaji huduma na maendeleo.
“Kenya ni familia moja, yenye utajiri wa utamaduni na maoni, na iliyounganishwa na mustakabali mmoja,” alisema Wetang’ula.
“Kuna wale ambao huamini kuwa wasipokuwa uongozini, taifa haliwezi tekeleza majukumu yake. Kuna nafasi ya kila mmoja wetu kutoa huduma zake popote alipo,” aliongeza Spika huyo.
Kulingana na Spika huyo, maendeleo ya taifa hili hutegemea na jinsi viongozi hushirikiana pamoja.