Serikali yazindua utoaji wa chanjo dhidi ya Surua,Rubella na Homa ya Matumbo

Tom Mathinji and Radio Taifa
2 Min Read
Aden Duale

Waziri wa afya Aden Duale leo Jumamosi, alizindua rasmi kampeni ya utoaji chanjo ya pamoja dhidi ya magonjwa ya  Surua, Rubella na homa ya matumbo kwenye uwanja wa Githogoro,Westlands, kaunti ya Nairobi.

Mpango huo wa kuokoa maisha unadhamiriwa kupiga jeki shughuli za utoaji chanjo na kukabili mzigo wa maradhi yanayoweza kuzuiwa kote nchini.

Akiongea katika hafla hiyo, Duale alikariri kujitolea kwa serikali kulinda afya ya watoto na jamii kwa jumla, akitoa wito kwa wazazi, walezi, walimu na viongozi wa kidini kuunga mkono kampeni ya utoaji chanjo kote nchini.

Alisisitiza kwamba chanjo hizo ni salama, zenye ufanisi na kwamba zinatolewa bila malipo katika vituo vyote vya afya vya umma.

Kampeni hiyo ambayo inaanza leo hadi tarehe 14 mwezi huu, inawalenga watoto walio na umri wa miezi-9 hadi miaka minne kwa chanjo za Ukambi na Rubella, na watoto wenye umri wa miezi-9 hadi miaka-14 kwa chanjo ya homa ya matumbo.

Waziri huyo alisema kuwa mpango huo ni hatua muhimu katika kutokomeza vifo vya watoto vinavyoweza kuzuiwa, na kutoa chanjo kwa wote wanaolengwa.

Aidha Duale alielezea wasiwasi wake kuhusiana na idadi ndogo ya kupokea dozi ya pili ya chanjo za surua na Rubella, akisema kwamba kati ya mwezi Januari mwaka-2024 na Februari mwaka-2025, Kenya ilinakili yamkini visa elfu-3 na vifo-18 vya ukambi.

Waziri huyo alisema kampeni hiyo ni sehemu ya juhudi za  taifa hili za kuwachanja watoto ambao hawakuchanjwa wakati janga la COVID-19 , na kurejesha imani katika huduma za afya za kimsingi.

Aliongeza kwamba chanjo ni muhimu katika ajenda ya serikali ya utoaji huduma bora za afya kwa wote na kwa gharama nafuu.

Website |  + posts
TAGGED:
Share This Article