Wahadhiri wakaa ngumu, waapa kuendelea na mgomo hadi walipwe

Mahakama iliamuru jana Alhamisi kuwa serikali iwalipe wahadhiri wanaogoma malimbikizi ya shilingi bilioni 7.9. 

Dismas Otuke
2 Min Read

Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma kote nchini wameapa kuendelea na mgomo baada ya kuazimia kuwa watakubali tu malipo ya malimbikizi yao ya mshahara kwa mkupuo mmoja. 

Serikali ilitaka kuwalipa malimbikizi hayo ya kima cha shilingi bilioni 7.9 katika awamu mbili.

Lakini baada ya kutafuta ushauri wa wanachama wao, maafisa wa vyama vya UASU na KUSU waliibuka leo Ijumaa na kusema kamwe hawatakubali malipo hayo kutolewa kwa awamu mbili bali wanataka kulipwa kwa mkupuo mmoja.

“Wahadhiri wamesema hawatoi elimu kwa wanafunzi kwa awamu,” alisema Katibu Mkuu wa UASU Dkt. Constantine Wasonga wakati akiwahutubia wanahabari.

“Kwa hivyo wanataka fedha hizo zilipwe kwa mkupuo mmoja tena mara moja,” aliongeza Dkt. Wasonga wakati akisisitiza kuwa mgomo wao ambao umeingia siku ya 46 leo Ijumaa utaendelea hadi matakwa yao yatimizwe kikamilifu.

Katibu Mkuu wa KUSU Dkt. Charles Mukhwaya akiongeza kuwa shauku ya wahadhiri kukataa kulipwa kwa awamu mbili imetokana na hulka ya serikali kuwachezea shere kila baada ya kuingia kwenye makubaliano siku zilizopita.

Ilitarajiwa kuwa wahadhiri wangekubali malipo kwa awamu mbili na hivyo kusitisha mgomo ambao umelemaza masomo katika vyuo vikuu vya umma kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu.

Ilivyo sasa, itawabidi wanafunzi kuendelea kuhisi makali ya mgomo huo.

Mahakama iliamuru jana Alhamisi kuwa serikali iwalipe wahadhiri wanaogoma malimbikizi ya shilingi bilioni 7.9.

Wahadhiri wamekataa katakata kulipwa kwa awamu wakisimama kidete na kusema kuwa ni sharti mwafaka wa nyongeza ya mshahara wa mwaka 2025-2029 usainiwe na shilingi bilioni 7.9 zitolewe kabla ya kumaliza mgomo.

Yamkini maji yamezidi unga na mazungumzo kutibuka Ijumaa baada ya serikali kusema iko tayari kulipa shilingi bilioni 7.9 kwa awamu mbili ndani ya miaka miwili.

 

 

 

Website |  + posts
Share This Article