Usajili wa maafisa wa polisi sasa kuandaliwa Novemba 17

Wanaotaka kusajiliwa ni sharti watume maombi kwa kujaza fomu zilizo kwenye tovuti za www.nationalpolice.go.ke; www.kenyapolice.go.ke; www.administrationpolice.go.ke; www.dci.go.ke; www.mygov.go.ke au wazipate fomu hizo kwa kutembelea vituo vya Huduma Centre vilivyo karibu nao. 

Dismas Otuke
2 Min Read

Usajili wa kitaifa wa maafisa wa polisi, kiwango cha konstebo, sasa utaandaliwa tarehe 17 mwezi ujao wa Novemba.

Tangazo hilo jipya limetolewa na Huduma ya Taifa ya Polisi, NPS, ingawa halielezei idadi kamili ya maafisa wa polisi watakaosajiliwa.

Awali, Tume ya Taifa ya Huduma ya Polisi, NPSC, ilikuwa imetangaza kuajiriwa kwa maafisa 10,000 wa polisi.

Nalo tangazo la NPS limetolewa siku moja baada ya Mahakama ya Kusuluhisha Migogoro ya Wafanyakazi kuamuru kuwa NPSC haina mamlaka ya kuajiri, kutoa majukumu wala kuhamisha polisi; hivyo basi, haipaswi kuendesha usajili huo.

Usajili utaandaliwa katika vituo 422 kote nchini kati ya saa mbili asubuhi na saa kumi na moja jioni.

Wanaotaka kusajiliwa ni sharti watume maombi kwa kujaza fomu zilizo kwenye tovuti za www.nationalpolice.go.ke; www.kenyapolice.go.ke; www.administrationpolice.go.ke; www.dci.go.ke; www.mygov.go.ke au wazipate fomu hizo kwa kutembelea vituo vya Huduma Centre vilivyo karibu nao.

Aidha, wanaotuma maombi ni sharti wawe na alama ya D+ katika mtihani wa KCSE, kimo cha futi 5.3 kwa wanawake na futi 5.8 kwa wanaume, na wasiwe na rekodi ya uhalifu.

Usajili wa maafisa wa polisi, kiwango cha konstebo ulikuwa umeratibiwa kuanza kati ya Oktoba 3-9 mwezi huu, kabla ya kusitishwa na mahakama kufuatia kesi iliyowasilishwa na mwanasiasa John Harun Mwai, kupinga zoezi hilo kuendeshwa na NPSC.

Website |  + posts
Share This Article