Ajuza ashangaza wengi Isiolo, abeba vifaa vinavyoshukiwa kuwa mabomu hadi kituo cha polisi

Bruno Mutunga
2 Min Read
Ajuza abeba vifaa vinavyoshukiwa kuwa bomu hadi kituo cha polisi Isiolo / Picha ya awali

Ajuza mwenye umri wa miaka 71 kutoka kijiji cha Kambi ya Juu, pembezoni mwa mji wa Isiolo, jana Alhamisi aliwashangaza maafisa wa polisi na wakaazi baada ya kufika katika kituo kidogo cha polisi cha Kambi ya Juu akiwa amebeba gunia lililokuwa na vifaa viwili vinavyoshukiwa kuwa mabomu ambayo hayajalipuka.

Tukio hilo limezua taharuki miongoni mwa wakazi na viongozi wa eneo hilo, ambao sasa wanaitaka serikali kuchukua hatua za haraka kufanya uchunguzi na usafishaji wa kina wa eneo hilo, ili kuhakikisha hakuna mabaki mengine ya mabomu ambayo yanaweza kuhatarisha maisha ya wakazi, hasa watoto wakati huu wa likizo ndefu.

Severina Kairigo amesema alipata vifaa hivyo viwili vikiwa vimeegemea karibu na kila kimoja alipokuwa akijiandaa kulima shamba lake dogo.

Kwa mujibu wake, alivitambua mara moja kuwa ni vitu hatari na akaamua kuviweka kwenye gunia na kuvipeleka kwenye kituo cha polisi, kwa hofu kwamba mjukuu wake anayesoma darasa la nane pamoja na watoto wengine wa kijijini wangevichezea.

Alisema aliweza kuvibaini kwa urahisi kwani miaka michache iliyopita, alikuwa ameona kifaa kingine kama hicho katika eneo hilo, na wakati huo aliwataarifu wanajeshi wa KDF waliokuwa wakipita kuelekea Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi cha KDF kilicho umbali wa kilomita chache kutoka kijijini hapo.

Wanajeshi walichukua kifaa hicho na kukilipua.

Wakazi wa eneo hilo wakiongozwa na meneja wa eneo, David Mwirigi, pamoja na kiongozi wa kidini Mchungaji Shadrack Ntoitha, wameiomba serikali ya Kenya kuchukua hatua za haraka kuhakikisha eneo hilo linachunguzwa kwa kina ili kubaini kama kuna mabaki mengine ya mabomu yaliyosalia na kuyaondoa kwa usalama wa jamii.

Inadaiwa kuwa vifaa hivyo viwili huenda ni mabomu ya ardhini yaliyosalia tangu enzi za ukoloni.

Hata hivyo, kutokana na uwepo wa kambi kadhaa za kijeshi katika kaunti ya Isiolo, baadhi ya wakazi wanashuku kuwa huenda mabaki hayo yanatokana na mazoezi ya kijeshi yaliyofanyika hapo awali.

Vifaa hivyo viwili viliwekwa katika uwanja wa kituo cha polisi usiku kucha, vikisubiri wataalamu wa mabomu kufika kuvichunguza na kuvilipua kwa usalama.

Bruno Mutunga
+ posts
Share This Article