Naibu Rais Rigathi Gachagua atafika mbele ya bunge la Seneti Alhamisi wiki hii kujitetea baada ya mahakama kuu kutupilia mbali ombi lake la kuzuia bunge hilo kusikiza mashtaka dhidi yake.
Jaji Chacha Mwita kwenye uamuzi wake Jumanne alasiri, amesema Seneti iko huru kusikiza na kubaini hatima ya mashtaka 11 yanayomkabili Naibu Rais.
Hilo ni pigo kubwa kwa Gachagua ambaye pia amewasilisha mahakamni kesi ya kupinga kubanduliwa kwake madarakani.
Jaji Mkuu Martha Koome tayari ameteua jopo la majaji watatu kusikiza kesi hiyo.
Bunge la Seneti sasa linatarajiwa kusikiza mashtaka dhidi ya Gachagua kesho na keshokutwa Alhamisi katika kikao cha Maseneta wote.
Kisha Maseneta watapigia kura kila shtaka katika hatua ambayo itaamua hatima ya Gachagua.
Wiki iliyopita, bunge la kitaifa lilipiga kura kuunga mkono hoja maalum ya kumng’atua afisini Naibu Rais kwa kukiuka sheria.
Wabunge 281 waliunga mkono hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.