Wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi watakiwa kurejea kazini mara moja

Martin Mwanje
2 Min Read

Wahadhiri wanaogoma wa Chuo Kikuu cha Nairobi, UoN wametakiwa kurejea kazini mara moja. 

Wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma kwa kipindi cha wiki tatu zilizopita wamekuwa wakigoma kushikiniza serikali kutimiza ahadi yake ya kuwaongezea mshahara kwa asilimia kumi kama ilivyokubaliwa katika makubaliano ya awali ya kurejea kazini.

Huku akikiri kuwa masuala yaliyoibuliwa na wahadhiri hao yana uzito, Makamu Chansela wa UoN Prof. Margaret Hutchinson amelalamikia namna mgomo huo ulivyolemaza masomo chuoni hapo.

Sasa anawataka hasa wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi kurejea kazini wakati mzozo wao ukishughulikiwa mahakamani.

“Mgomo huo umeathiri siyo tu masomo lakini pia umeathiri utafiti, huduma za jamii na shughuli zote za chuo kikuu,” amesema Prof. Hutchinson katika taarifa.

“Mgomo huo umewasilishwa mahakamani na kutajwa kuwa usiokuwa halali. Tunavyozungumza, mgomo huo unashughulikiwa na kamati ya mazungumzo kati ya wizara, na nina imani masuala yanayozozaniwa yatasuluhishwa kwa amani hivi karibuni.”

Kwa maelezo zaidi kuhusu hotuba ya Prof. Hutchinson kwa jumuiya ya UoN, tazama video ifuatayo:

YouTube player

Prof. Hutchinson amesisitiza kuwa ni muhimu kwa Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, UASU kuendelea na mazungumzo ili kuutafutia mgomo huo ufumbuzi.

Amewataka wahadhiri wa UoN kurejea kazini mara moja la sivyo wataadhibiwa kwa mujibu wa sheria na mikataba yao ya kuajiriwa.

Chama cha UASU kimeapa kuwa wahadhiri wa vyuo vikuu vya umma hawatarejea kazini hadi matakwa yao yatimizwe.

 

Share This Article