Waandamanaji watakiwa kutoenda maeneo yasiyoruhusiwa

Martin Mwanje
1 Min Read

Vijana wa Gen Z waliopanga kufanya maandamano leo Jumanne wametakiwa kuhakikisha hawaandamani kuelekea maeneo yasiyoruhusiwa kisheria.

Kaimu Inspekta Mkuu wa Polisi Douglas Kanja amelihakikisha taifa kujitolea kwa serikali kuhakikisha usalama wa umma na taifa wakati wa maandamano hayo.

“Kwa kuzingatia maandamano yaliyopangwa kufanywa Julai 23, 2024, ni muhimu kuukumbusha umma mipaka ya kisheria inayosimamia maeneo yanayolindwa,” alisema Kanja katika taarifa.

“Sheria ya maeneo yanayolindwa kifungu cha 204 cha sheria za Kenya inazuia watu wasioruhusiwa kuingia maeneo ambayo yametangazwa kuwa yanayolindwa.”

Ametaja maeneo hayo kuwa yanayojumuisha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta, JKIA.

Vijana wa Gen Z wameripotiwa kutishia kuingia katika uwanja huo na kutatiza shughuli uwanjani hapo.

Hata hivyo, usalama umeimarishwa maradufu katika maeneo hayo ikiwa ni pamoja na majengo ya bunge na Ikulu ya Nairobi wakati vijana hao wakipanga kuandamana leo Jumanne.

Share This Article
Leave a Comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *