Viongozi wamiminika Mwanza harusi ya Charlene Ruto

Harusi hiyo ya kufana ilifanyika katika mkahawa wa kifahari wa Malaika Beach Resort jijini Mwanza nchini Tanzania.

Martin Mwanje
2 Min Read

Viongozi mbalimbali wa serikali jumuishi, wakiwemo mawaziri, walitua jijini Mwanza nchini Tanzania leo Ijumaa kuhudhuria harusi kati ya Charlene Ruto, ambaye ni mwanawe Rais William Ruto na mpenziwe, Isaya Yunge. 

Waliohudhuria harusi hiyo iliyofanyika katika mkahawa wa kifahari wa Malaika Beach Resort ni pamoja na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi na Mawaziri Aden Duale wa Afya na Kipchumba Murkomen wa Usalama wa Taifa.

Wengine ni Magavana Gladys Wanga wa Homa Bay na Stephen Sang wa Nandi.

Katika mitandao ya kijamii, nadhari ilielekezwa katika jiji la Mwanza huku wengi wakifuatilia mandhari na ilivyofanyika harusi hiyo.

Akizungumza kabla ya hafla ya wawili hao kufunga ndoa leo Ijumaa, Rais Ruto alimsifia Yunge akimtaja kuwa jasiri na kumhakikishia kuwa watamchukulia kama mtoto wao.

Alielezea matumaini kwamba ndoa kati yao itafana.

Kisha Ruto na mkewe, Rachel, walitembea asteaste kumkabidhi binti yao kwa mkwe wao wakati nyuso zao zikifunikwa na wingu la tabasamu wakati binti yao akiasi useja.

Mioyoni, waliwatakia wanandoa hao mema wanapofungua ukurasa mpya maishani.

Charlene aliwasili jijini Mwanza juzi Jumatano akitumia ndege ya kibinafsi kabla ya kusafirishwa na msafara wa magari ya kifahari hadi hotelini.

Novemba 3, 2026, binti huyo aliandaliwa hafla ya kumfunza mawili matatu kabla ya kufunga ndoa ambapo wahudhuriaji walivaa mavazi ya rangi nyeupe na kahawia.

Awali, Charlene na Isaya walifanya sherehe ya mahari na kuvishana pete za uchumba Agosti 8, 2026 nyumbani kwa Rais Ruto huko Kilgoris, kaunti ya Narok nchini Kenya.

Sherehe hiyo ya uchumba iliwakutanisha ndugu na jamaa wa pande zote mbili, ikiwa ni sehemu ya taratibu za kimila kabla ya wawili hao kuingia rasmi kwenye ndoa.

Sasa wengi wanaangazia jiji la Mwanza, ambako familia hizo mbili kwa mara nyingine zitaungana katika harusi ya wanao.

Tunawatakia wawili hao kila la heri wanapoanza maisha pamoja kama wanandoa.

Share This Article