Rais William Ruto amekabidhi Chuo Kikuu cha Kamagambo barua ya muda ya utendaji kazi.
Kiongozi wa taifa alisema Chuo hicho kikuu kitabuni fursa za elimu ya juu kwa vijana kutoka kaunti ya Migori na taifa nzima kwa jumla, huku kikitoa mafunzo kwa walimu, wajasiriamali na wataalam wanaohitajika kupiga jeki mageuzi ya kiuchumi ya taifa hili.
“Tunahimiza usimamizi wa Chuo Kikuu hiki kuzingatia viwango vya ubora vya hali ya juu na uongozi mwafaka, kinaposubiri kuwa Chuo Kikuu kamili,” alisema Rais Ruto kwenye hafla iliyoandaliwa katika Ikulu ndogo ya Kisumu Jumanne asubuhi.
Rais alisema ili kupanua upatikanaji wa elimu ya juu nchini Kenya, serikali inafanyia mabadiliko mfumo wa kuwachagua wanafunzi na ufadhili wa elimu ya Vyuo Vikuu, Taasisi za Kiufundi na Taasisi ya Mafunzo ya Utabibu kupitia mswada wa elimu ya juu na ufadhili wa mwaka 2026.
Aidha, alidokeza kuwa Vyuo Vikuu haviimarishi tu taasisi na kutekeleza utafiti, lakini pia zinatatua changamoto na kubuni mawazo yanayochipuza viwanda vipya.
“Chuo Kikuu ni mahali ambapo mawazo yanakuzwa ambayo yataunda mustakabali unaohitajika,” alisema Rais Ruto.
Alisema serikali imeongeza bajeti ya kitaifa ya elimu kwa zaidi ya shilingi bilioni 200, hii ikiwa ni ongezeko kutoka shilingi bilioni 500 mwaka 2022, hadi shilingi bilioni 702 mwaka huu wa kifedha 2026/2027.