Raia wa Kenya waendelea kurejeshwa salama kutoka Afrika Kusini

Wakenya 151 tayari wamewasili nchini kupitia safari za ndege za Kenya Airways kati ya Juni 30 na Julai 1.

Marion Bosire
2 Min Read
Musalia Mudavadi - Mkuu wa Mawaziri.

Serikali ya Kenya imeongeza juhudi za kuwarejesha nyumbani raia wake walioko Afrika Kusini kufuatia ongezeko la wimbi la mashambulizi ya chuki dhidi ya wageni na vitendo vya vitisho vinavyolenga raia wa kigeni.

Katika taarifa iliyotolewa Alhamisi, Mkuu wa Mawaziri ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje Musalia Mudavadi, alisema zoezi la kuwaondoa raia hao linafanyika kwa utaratibu, usalama na kwa wakati ili kuwalinda Wakenya walioathiriwa na machafuko hayo.

Mudavadi alisema kwamba jana, Julai 1 alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri wa Mahusiano ya Kimataifa na Ushirikiano wa Afrika Kusini, Roland Lamola, ambaye aliihakikishia Kenya kuwa serikali ya Afrika Kusini inaendelea kuchukua hatua zote muhimu kuhakikisha usalama wa raia wa kigeni, wakiwemo Wakenya.

Ubalozi Mkuu wa Kenya mjini Pretoria unaratibu zoezi hilo kwa ushirikiano na mamlaka za Afrika Kusini, huku Wizara ya Mambo ya Nje ikiratibu usafiri wa ndani, safari za ndege kuelekea Nairobi, utoaji wa hati za dharura za usafiri na misaada ya kibinadamu kwa wanaotaka kurejea nyumbani.

Kufikia Julai 2, 2026 jumla ya Wakenya 240 walikuwa wamejisajili wakiomba msaada, huku ubalozi ukiwapatia makazi ya muda, chakula, mahitaji muhimu na huduma maalum kwa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, wakiwemo watoto wachanga.

Wakenya 151 tayari wamewasili nchini kupitia safari za ndege za Kenya Airways kati ya Juni 30 na Julai 1. Kundi jingine la watu 55 lilitarajiwa kuwasili baadaye Alhamisi.

Licha ya ghasia hizo, serikali ilisema kuwa idadi kubwa ya takribani Wakenya 27,000 wanaoishi Afrika Kusini wako salama na wanaendelea kuchangia maendeleo ya uchumi wa mataifa yote mawili.

Kenya pia iliishukuru serikali ya Afrika Kusini kwa ushirikiano wake na kusisitiza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.

Share This Article